MAONI: 'Bara la Ulaya ni mshirika wa Afrika, katika kujenga mustakabali wa pamoja' na Josep Borrell
Wiki hii niko safarini barani Afrika; bara lenye uchangamfu linalojiandaa na kesho yake; likisukuma mabadiliko ya kidijitali, likiboresha kilimo na kukifanya endelevu, kujenga miundombinu mipya ili kuwezesha utangamano kati ya watu, kujenga usalama shirikishi wa bara zima, na kuwekeza katika rasilimali kuu ya Afrika: vijana wake.
Katika haya yote, tunapendekeza Ulaya awe mshirika teule wa Afrika.
Uwekezaji wa Ulaya barani Afrika ni mara tano zaidi ya ule wa Uchina. Robo ya biashara ya Afrika ni kati yake na Umoja wa Ulaya; ni asilimia 15 pekee na Uchina na asilimia mbili na Urusi. Asilimia 90 ya bidhaa za Afrika huingia kwenye soko la Umoja wa Ulaya (EU) bila kulipishwa. EU pia imekuwa ikishirikiana na Afrika kujenga viwanda vya kutengeneza chanjo ya magonjwa mbalimbali kwa kima cha Euro 150 bilioni ; ukiwa mradi wa kwanza aina yake kuanzishwa Afrika. Mataifa ya EU pia yamekuwa yakichangia kueneza amani kwenye mataifa ya Afrika ambayo yamekuwa yakikabiliwa na vita au mapigano yanayosababisha ukosefu wa serikali thabiti.
Hata hivyo, vita kati ya Urusi na Ukraine ni kati ya mambo ambayo yameathiri uhusiano wa EU na Afrika, hali kadhalika na mabara mengine. Vita hivyo, vimechangia kupanda kwa gharama za maisha kwa kuwa nchi za Afrika zinategemea bidhaa muhimu kutoka nchi hizo mbili. Kwa mfano, bei ya mafuta imepanda na mataifa ya Afrika yaliyokuwa yakiwasilisha bidhaa zao katika nchi hizo mbili, yamekosa soko kutokana na misukosuko iliyokwepo. Japo tunaelewa kuwa baadhi ya nchi za Afrika wanamitazamo tofauti juu ya vita hii, ninadhani tunaweza kukubaliana katika hoja nne za msingi.
Mosi: EU, Afrika na mabara mengine hayawezi kukubali mataifa makubwa yaingilie mipaka ya nchi ndogo na hilo linarejesha kumbukumbu za kabla ya uhuru ambapo nchi za Afrika zilikuwa chini ya Wakoloni. Kwa hivyo, EU inapinga hatua ya Urusii kuingilia Ukraine. Wananchi wa Ulaya wanaelewa vyema majukumu yao katika karne hiyo, na hivyo EU imedhamiria kupinga marudio ya ukoloni. Ni lazima tuendeleze na kutilia nguvu makubaliano ya kongamano la majuzi kati ya EU na Afrika, kulinda utawala wa sheria kama ilivyokubaliwa. Hiyo ndiyo sababu kuu kwa nini EU inaunga wito wa Rais Sall kwamba Umoja wa Afrika uwe na kiti katika G20.
Pili: Lazima tuchukue hatua kupunguza mzozo kuhusu chakula. Ikiwa na zaidi ya washirika 70, wengi wakiwa Afrika, EU inachukua hatua katika vitengo vinne; kusimama na wasioweza kupata chakula, kuunga uzalishaji chakula, kuwezesha kilimo biashara ikiwa pamoja na kufikisha nafaka za Ukraine barani Afrika; na kuainisha jinsi tunavyoshughulikia wito wa kusambaza chakula katika mifumo yetu na Umoja wa mataifa.
Wengine wanajaribu kukwepa jukumu lao kwa kulaumu vikwazo. Hata hivyo, ukweli uko wazi. Vikwazo vya EU havijazuia nchi za Afrika kuagiza au kusafirisha chakula na bidhaa za mazao kutoka Urusi, au kuzilipia. Vita vya Urusi ndio tatizo wala si vikwazo. Iwapo washirika wetu Afrika wanakumbwa na changamoto katika kununua au kuingiza bishaa za chakula kutoka Urusi kutokana na vikwazo vyetu, tutashirikiana kushughulikia tatizo hilo.
Tatu: Tunapaswa kuongeza juhudi za kuimarisha usalama Afrika. Katika suala hili, EU ndiye mshirika wa kutegemewa na Afrika, ikiunga mkono juhudi za amani katika nchi 11 za Afrika ambazo zinakabiliwa na mizozo ya kisiasa. Mnamo Aprili, EU ilitoa Euro milioni 600 kusaida Afrika kupambana na ugaidi, kutatua mizozo ya kisiasa na kuzuia mapigano ya ndani kwa ndani. Wiki hii nitakuwa Msumbiji na Somalia. Kule Msumbiji, EU ilituma majeshi yake ambayo yamekuwa yakidumisha usalama katika mkoa wa Cabo Delgado huku ikitumia Euro 89 milioni kwa shughuli hiyo. EU pia imetumia Euro bilioni 2.3 kuimarisha majeshi ya kulinda amani ya AU ambayo yamekuwa yakilinda usalama nchini Somalia kwa zaidi ya miaka 10.
EU hujitolea wanausalama 6000 katika vikosi vya kudumisha amani Afrika vya Umoja wa Mataifa (UN) huku Urusi ikitoa 78 pekee. Pia, Urusi imekashifiwa kwa kuchangia udororaji wa usalama barani Afrika kutumia mamia ya mamluki wa usalama wanaokudishwa kwenye majeshi binafsi kama Wagner au Patriot. Uwepo wao unazidi kuzorotesha usalama na haki za kibinadamu, kama ilivyojitokeza Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Nne: Afrika na Ulaya wanapaswa kujizatiti katika kuandaa mustakabali bora zaidi badala ya kusalia katika historia. Kuna baadhi wanaojaribu kutugawanya kwa kuibua yaliyopita, huku wakipuuza hatua tulizopiga kwa pamoja kwa miongo kadhaa.
Ukoloni ni doa lisilofutika katika historia ya Ulaya, lakini kuwajibika na makosa hayo kumetufanya kuwa washirika bora. Ulaya inaitazama Afrika kwa macho mapya: kwa matumaini na kujiamini. Hiyo ndiyo sababu ya kutaka kuimarisha ushirikiano wetu, daima tukitanguliza azma ya “Ufumbuzi wa kiafrika kutatua matatizo ya Afrika”.
Hata hivyo, wengine wanaonekana kushawishika kurudia makosa yaliyofanywa na Wazungu, kwa kutaka kuiba maliasiili ya Afrika, kudhibiti ardhi na kilimo, kuzifanya nchi za Afrika tegemezi wa misaada ya kifedha, au kujaribu kutumia nguvu za vijana wa Afrika kwa manufaa yao ya binafsi.
Sisi huku Ulaya tunapojizatiti kuimarisha kujitegemea kiuchumi kwa EU, tunaunga mkono Afrika kufanya vivyo hivyo. Lazima sote tushirikiane na wadau mbalimbali, tukiheshimiana na kuzingatia sheria za kimataifa. Hizi ndizo kanuni za Karne ya 21. Katika mfumo huo, Afrika na Ulaya tunapaswa kuimarisha mahusiano na ushirikiano wetu kwa sababu mustakabali wenu ni mustakabali wetu pia.
*Borrell ni Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu masuala ya kigeni na usalama