Ujumbe wa Ufuatiliaji wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya unatoa wito kwa mamlaka za Kenya kuharakisha mageuzi ya uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2027 unakuwa wazi, shirikishi, na wa amani

Ujumbe wa Ufuatiliaji wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya unatoa wito kwa mamlaka za Kenya kuharakisha mageuzi ya uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2027 unakuwa wazi, shirikishi, na wa amani.

Umoja wa Ulaya ulituma Ujumbe wa Ufuatiliaji wa Uchaguzi (EU EFM) kwa Jamhuri ya Kenya kuanzia tarehe 2 Februari hadi 1 Machi 2025, ili kutathmini maendeleo yaliyofanyika katika mchakato wa mageuzi ya uchaguzi na hali ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Ujumbe wa Uangalizi wa Uchaguzi wa EU 2022 (EU EOM 2022). Ujumbe huu wa Ufuatiliaji wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EFM) unaongozwa na Bw. Ivan Štefanec, aliyekuwa Mwangalizi Mkuu wa Ujumbe wa Uangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) mwaka 2022 na aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Ulaya.


Ujumbe wa Ufuatiliaji wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EFM) unathamini uhusiano mzuri na mazingira ya kirafiki wakati wa mikutano na idadi kubwa ya wadau katika mchakato wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), taasisi husika za serikali, vyama vya kisiasa, asasi za kiraia, wawakilishi wa vyombo vya habari, na washirika wa maendeleo. Mnamo tarehe 20 Februari, ujumbe huu uliandaa mkutano wa meza ya duara wa wadau wa uchaguzi, ambapo washiriki walijadili maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa katika utekelezaji wa mapendekezo ya EU EOM ya mwaka wa 2022 na hali ya sasa ya mageuzi ya uchaguzi.


Katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Nairobi, Bw. Štefanec alisema: "Kuna hatua chanya katika maeneo fulani, kwani majadiliano kuhusu mageuzi ya uchaguzi yameanza. Hata hivyo, tulibaini ukosefu wa maendeleo ya wazi katika utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Ujumbe wa Uangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya EU, EOM katika mwaka 2022. Wengi wa wale tuliowasiliana nao walikubaliana juu ya umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inayojitegemea na inayojiendesha kikamilifu kabla ya uchaguzi ujao."


Mnamo mwaka wa 2022, Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) ulitoa mapendekezo 21, yakiwemo mapendekezo saba yaliyopewa kipaumbele, kulingana na uchunguzi, uchambuzi, na majadiliano na wadau mbalimbali. Mapendekezo hayo yalijumuisha, miongoni mwa mengine, kutoa fedha za kutosha kwa IEBC kwa ajili ya elimu endelevu ya wapiga kura, kuboresha teknolojia ya uchaguzi kupitia ukaguzi wa mara kwa mara na mashauriano na wadau, kuwezesha utekelezaji wa Sheria ya Ufadhili wa Kampeni za Uchaguzi ili kudhibiti matumizi ya kampeni kwa ufanisi, kufafanua kisheria maana ya matamshi ya chuki kulingana na wajibu wa kimataifa wa haki za binadamu, kuondoa vifungu vya 22 na 23 vya Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni, na kuanzisha taratibu wazi za usimamizi wa wafanyakazi na mtiririko wa taarifa katika vituo vya kuhesabu kura ili kuongeza uthabiti na ufanisi wa mchakato wa uchaguzi.


Bwana Ivan Stefanac alisema: “Kucheleweshwa kwa uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC kumepelekea kuahirishwa kikamilifu kwa chaguzi ndogo zinazosubiri, kusimamishwa kwa uwekwaji wa mipaka, kusitishwa kwa usajili endelevu wa wapiga kura, na kuathiri maandalizi ya jumla ya uchaguzi wa mwaka 2027. Ni muhimu kwamba IEBC iundwe upya bila kuchelewa zaidi na ipewe ufadhili wa kutosha na kwa wakati ili kujiandaa kwa uchaguzi wa mwaka 2027.”
 

Bwana Štefanec alisisitiza umuhimu wa kuwezesha raia wote kujiandikisha kama wapiga kura, kutumia haki yao ya kupiga kura na kugombea nafasi, sambamba na ahadi za kimataifa na kikanda za Kenya. Alisisitiza haja ya kuweka imani katika kazi ya IEBC, kuimarisha uhuru wake, kuhakikisha uwazi katika mchakato wa uchaguzi, huku ushirikishwaji na ushirikiano vikikuzwa miongoni mwa wadau wa uchaguzi.
Akihitimisha mkutano na waandishi wa habari, Bwana Štefanec alisisitiza kuwa EU na Nchi Mwanachama zitaendelea kutetea mageuzi ya uchaguzi nchini Kenya.


Ripoti ya kina ya mwisho ya Ujumbe wa Ufuatiliaji wa Umoja wa Ulaya (EU) itachapishwa katika miezi ijayo.


Ripoti ya mwisho ya Ujumbe wa Uangalizi wa Umoja wa Ulaya inaweza kupatika hapa:
https://www.eeas.europa.eu/sites/default/files/documents/EU_EOM_Kenya_2022_EN.pdf