Delegation of the European Union to the African Union

UZINDUZI WA MAGHALA YA KUHIFADHIA NAFAKA MKOANI MOROGORO KWA UFADHILI WA UMOJA WA ULAYA (EU)

Tanzania, 13/09/2019 - 10:53, UNIQUE ID: 190913_3
Joint Press Releases

Alhamisi, 12 Septemba 2019, Kilosa – Morogoro: Mkuu wa Wilaya ya Kilosa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU) na Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la HELVETAS wamezindua maghala sita ya kuhifadhia nafaka ambayo yamejengwa au kukarabatiwa na Mradi wa Kupunguza upotevu wa Mpunga wakati na baada ya mavuno (RIPOMA), maghala hayo yapo wilaya ya Kilosa na Mvomero na yanawanufaisha zaidi ya wananchi 15,000.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU) na Mkurugenzi  Msaidizi wa Shirika la HELVETAS wamezindua maghala sita ya kuhifadhia nafaka ambayo yamejengwa au kukarabatiwa na Mradi wa Kupunguza upotevu wa Mpunga wakati na baada ya mavuno (RIPOMA), maghala hayo yapo wilaya ya Kilosa na Mvomero na yanawanufaisha zaidi ya wananchi 15,000. Uzinduzi huu ulihudhuriwa pia  na wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo pamoja na  Wizara ya Afya. Wengine waliohudhuria ni maafisa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Halimashauri za Wilaya na wawakilishi kutoka SIDO, HELVETAS, DBB, JRT na maafisa mradi kutoka Shirika la CODERT, wakulima na wananchi kwa ujumla.

Maghala haya yamegarimu takribani TZS 508.56M (EUR 200,000) hii ilikuwa ni moja ya shughuli muhimu za Mradi wa Kuwawezesha Wakulima wadogo (Wanawake na Vijana) kupunguza upotevu wa Mpunga wakati na baada ya mavuno (RIPOMA). RIPOMA ni mradi wa miaka mitatu (Julai 2017 mpaka Juni 2020 wenye bajeti ya EUR 1,875,000 (takribani. TZS 4.768 Bilion) ambapo Umoja wa Ulaya (EU) umechangia 80% na HELVETAS 20%.  HELVETAS inatekeleza mradi huu kwa kushirikiana na Community Development and Relief Trust (CODERT), Small Industries Development Organisation (SIDO), JRT Agri-services (JRT), DBB Agro-Initiative, Halimashauri za Wilaya na Serikali ya Tanzania.

Mradi wa RIPOMA unakusudia kushughulikia changamoto zinazokabili  kilimo cha mpunga nchini hususan tija ndogo, upungufu wa mazao, upotevu mkubwa kabla na baada ya mavuno,  uwezo mdogo wa utunzaji na usindikaji, vikwazo katika kupata huduma za kifedha na mikopo, kutokuwepo kwa soko la uhakika na uhusiano dhaifu katika mfumo soko. Mradi umenufaisha kaya 3005 kwa kupitia vikundi 101 vya wakulima wanawake na vijana katika vijiji 36. Wawakilishi wa kaya hizo wamepewa mafunzo  ya kilimo bora, usimamizi wa mazao wakati na baada ya mavuno na kuongeza thamani, kuweka na kukopa, ubora na kukidhi vigezo vya masoko, usimamizi na uendeshaji wa vikundi, ushirika na maghala, pia tafiti za masoko, ziara za mafunzo na kushiriki maonesho ya kibiashara.

 

Katika hotuba yake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dr. Stephen Kebwe alisema, “ Napenda kuwahakikishia HELVETAS na Umoja wa Ulaya kuwa Serikali ya Mkoa itahakikisha wilaya husika zinaendelea kusaidia utekelezaji wa mradi na maafisa ugani wa kilimo wataendelea kutoa huduma bora za mafunzo kwa wakulima.” Maghala haya yatapunguza upotevu wa mpunga. Pia yatawezesha kuwa vituo vya kukusanyia kwa ajili ya kuuza kwa pamoja ili kupata bei nzuri na njia rahisi ya kupata mikopo kupitia Banki, aliongezea Mkuu wa Wilaya.

 

Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Bi. Anna Costantini wakati wa uzinduzi alisema: “Katika Mradi huu, Umoja wa Ulaya na HELVETAS, wamechangia kukuza  sekta ya mpunga  Morogoro. Ni matumaini yetu kuwa mbegu iliyopandwa na Mradi wa RIPOMA itaendelea kukua, pia nashukuru kwa ushirikiano ulioanzishwa na halimashauri za wilaya, taasisi za utafiti na mafunzo na sekta binafsi, pamoja na  msaada mpana ambao Umoja wa Ulaya utaendelea kuutoa katika kilimo Nyanda za juu Kusini.”

 

Mkurugenzi Msaidizi wa HELVETAS Bwana. Daniel Kalimbiya alisema, “Ni matarajio yangu kuwa maghala haya yatatunzwa  na kutumiwa kikamilifu na jamii na Serlikali ili kuongeza kipato, usalama wa chakula na lishe, na pia kutumia njia na teknolojia na kuzuia upotevu. Pia nawashukuru Umoja wa Ulaya (EU), Halimashauri za wilaya na Serikali kuu, na wadau kwa kuwawezesha wakulima wadogo hususan wanawake na vijana.

 

Mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo Bw. Beatus Malema alisema, “Maghala haya  ni nyenzo muhimu sana kwa wakazi wa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya usalama wa chakula, kuongeza kipato na kupata huduma za kifedha kupitia mfumo wa Stakabadhi Ghalani.

 

Baadhi ya mafanikio makubwa ya mradi hadi sasa ni pamoja na: tija imeongezeka kutoka gunia 10-15 hadi 25-40 kwa ekari kwa sababu ya mbinu bora za kilimo. Mafanikio haya yamesaidia kuongezeka kwa kipato na usalama wa chakula kwa sababu ya kutumia teknolojia za kuzuia upotevu wa mavuno, kuongezeka kwa upatikanaji wa fedha na fursa zaidi za kujiajiri kwa wanawake na vijana.

 

Mmoja wa wanufaika wa Mradi kutoka Dihombo alisema “Nashukuru sana  usaidizi wa Mradi wa RIPOMA, nimeweza kusomesha watoto wangu wawili na mmoja kwa sasa ameweza kwenda Chuo Kikuu kusomea Uhandisi na mmoja anamalizia Elimu ya Sekondari." Pia mnufaika mwingine kutoka Hembeti alisema kuwa ameongeza mara tatu ukubwa wa duka lake kwa kupata mtaji kupitia mradi wa RIPOMA.

 

Wakulima wadogo ndio wawekezaji wakuu katika kilimo nchini Tanzania na nchi zinazoendelea, hususan bara la Afrika.

 

Usuli:

Sera ya Taifa ya Kilimo imebainisha kuwa mpunga ni zao lenye fursa kubwa ya kuongeza pato kwa Taifa na Wakulima. Takribani 25% ya uzalishaji wa mpunga kitaifa unatoka mikoa ya Mbeya na Morogoro.

 

Tafiti mbili zilizofanywa na HELVETAS zilibaini kuwa kilimo cha mpunga kwa sehemu kubwa kinafanywa na wakulima wadogo (wenye umri wa miaka 19-45). Utafiti huo pia uligundua kuwa umiliki wa mali, hasusan ardhi na zana za kilimo zinamilikiwa zaidi na wanaume, ingawa wanawake wanachangia 60-80% ya nguvu kazi katika kilimo. Matokeo kwa jumla yalionyesha kuwa wanawake na vijana wana jukumu kubwa katika kilimo cha mpunga na mahindi  hivyo jitihada za makusudi na za haraka zinahitajika katika kuwapa maarifa ya  ujasiriamali na ya kumiliki mali ili kukuza ajira  na kupunguza umaskini

 

Mradi wa RIPOMA ni mojawapo ya miradi mitatu yenye thamani ya EURO milioni 4.5 kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya inayotekelezwa na HELVETAS, Food and Agriculture Organization of the United Nations (FAO) na the Aga Khan Foundation (AKF) kusaidia mnyororo wa thamani wa mchele katika mikoa ya Morogoro na Iringa na kusaidia wakulima wadogo, hususan wanawake na vijana.

 

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU) na Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la HELVETAS wakifungua rasmi ghala mojawapo mjini Morogoro
Editorial Sections: